China imesema iko tayari “kupambanaa hadi mwisho” katika vita vya kibiashara na Marekani, baada ya Rais Donald Trump kutangaza ushuru wa asilimia 100 kwa bidhaa zote za China, hatua iliyotikisa masoko ya dunia.
China imesema iko tayari "kupambana hadi mwisho” katika vita vya kibiashara na Marekani, kufuatia tangazo la Rais Donald Trump kwamba ataweka ushuru wa ziada wa asilimia 100 kwa bidhaa zote kutoka China. Msemaji wa wizara ya biashara ya China alisema Jumanne kuwa msimamo wa nchi hiyo kuhusu vita vya ushuru unabaki uleule: "Mkitaka kupigana, tutapigana hadi mwisho; mkitaka mazungumzo, mlango uko wazi.” Kauli hiyo imeibua wasiwasi mpya kuhusu kuongezeka kwa mvutano kati ya uchumi mkubwa zaidi na wa pili kwa ukubwa duniani.
Tangazo la Trump lilitolewa Ijumaa, likitaja hatua hiyo kama majibu kwa uamuzi wa Beijing kuweka vikwazo vipya vya usafirishaji wa madini adimu — sekta muhimu duniani inayotawaliwa na China. Hatua hiyo imeutikisa ulimwengu wa biashara, huku wachambuzi wakionya kuwa vita vya kibiashara vinaweza kuathiri vibaya masoko ya hisa na mahusiano ya kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.