Mwili wa aliyekuwa Askofu KKKT Dk Martin Shao waagwa rasmi

Viongozi mbalimbali wameshiriki ibada ya kuaga mwili wa aliyekuwa Askofu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, Dk Martin Shao. 


Miongoni mwa viongozi hao yupo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko, mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, 

Ibada hiyo ya kuaga mwili imefanyika leo Jumatano, Septemba 4, 2025 katika Usharika wa Lole, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, na kuongozwa na Mkuu wa 

Kanisa la KKKT, Askofu Alex Malasusa.
Serikali iliwakilishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dotto Biteko, pamoja na viongozi wengine wa kitaifa na kimkoa, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Dk Martin Shao, ambaye alihudumu kama Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini kuanzia mwaka 2004 hadi alipostaafu mwaka 2014, alifariki dunia Agosti 25 mwaka huu wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, mjini Moshi.

Mwili wake unatarajiwa kuzikwa kando ya kanisa hilo, mahali ambapo aliwahi kulihudumia kwa miaka mingi, huku waombolezaji kutoka sehemu mbalimbali wakiendelea kumiminika kutoa heshima zao za mwisho.

Tukio hilo limewaweka pamoja viongozi wa kisiasa wa zamani na wa sasa, ikiwa ni ishara ya umoja mbele ya huzuni wa kuondokewa na kiongozi huyo. 

Mwalimu aliyeko mkoani hapo amelazimika kupeleka mbele ratiba ya mkutano wake wa muendelezo wa kampeni za kuomba kura ili achaguliwe na Umma kushika wadhifa huo Oktoba 29 mwaka huu.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii