Bwawa la JNHPP kuwa kielelezo cha ushirikiano maonyesho ya IATF2025

Mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere (JNHPP) katika Mto Rufiji, umetajwa kuwa kielelezo cha ushirikiano wa Bara la Afrika wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Nne ya Biashara ya Ndani ya Afrika (IATF2025) yanayofanyika jijini Algiers. 

Viongozi na maofisa waliokusanyika katika maonesho hayo ya wiki moja wanasema mradi huo wa Dola bilioni 2.9 unadhihirisha namna ushirikiano chini ya Mkataba wa Biashara Huria Afrika (AfCFTA) na taasisi za kifedha za kikanda unavyoweza kugeuza ndoto kubwa kuwa halisi.

Profesa Benedict Oramah, Rais na Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Maendeleo ya Uagizaji na Uuzaji Nje ya Afrika (Afreximbank), amewaeleza wajumbe kwamba wakati Tanzania ilipotangaza mpango huo wenye lengo la kuzalisha zaidi ya megawati 2,000 za umeme, kudhibiti mafuriko na kusaidia wakulima, wadau waliupokea kwa mashaka. “Taasisi za fedha za kimataifa, makampuni ya bima na wakandarasi walikataa kushiriki katika mradi huo,” amesema Oramah.

Hali ilibadilika mwaka 2018 wakati wa maonesho ya kwanza ya IATF yaliyofanyika Cairo, Misri, ambapo Tanzania ilisaini mkataba wa ujenzi na makampuni ya Misri, Arab Contractors na El-Sewedy Electric. 


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii