Afreximbank yataka mapambano mapya ya kiuchumi

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Uagizaji na Uuzaji Nje ya Afrika (Afreximbank), Profesa Benedict Oramah, amewataka viongozi, wawekezaji na wafanyabiashara barani Afrika kuendeleza “mapambano mapya” ya ukombozi wa kiuchumi kupitia biashara, ubunifu na viwanda.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Biashara ya Ndani ya Afrika (IATF2025) jijini Algiers, Oramah alilinganisha harakati hizo na mapambano ya kupata uhuru wa kisiasa yaliyotokea miaka ya 1960. “Badala ya kupigana vikumbo, vita hivi sasa tupiganie kukuza viwanda na vituo vya ubunifu wa teknolojia… tunajitaji kuwa jasiri kwa kuwa ni muhimu kwa mapambano ya kiuchumi,” amesema.

Oramah alieleza kuwa IATF imekuwa jukwaa la kugeuza ndoto kuwa miradi mikubwa. Alitaja mfano wa mradi wa Dola bilioni 2.9 wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) nchini Tanzania, uliotekelezwa baada ya taasisi za kimataifa kuukataa. Mradi huo sasa unazalisha megawati 2,115 na kuiwezesha Tanzania kujitegemea kwa umeme.

Aliongeza kuwa mafanikio mengine yaliyotokana na IATF ni pamoja na kiwanda cha kusindika samaki Mauritania, hoteli ya kifahari ya Galawa visiwani Comoro, na uwekezaji wa dola milioni 450 kwa ujenzi wa kongani ya viwanda katika nchi sita.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii