Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limefanya matengenezo kinga kwenye njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa Kilovoti 220 kutoka kituo cha kupoza umeme cha Chalinze hadi Kinyerezi Dar es Salaam bila kuzima umeme.
Matengenezo hayo yalihusisha ubadilishaji wa vikombe (insulator) ambavyo vilionekana kuwa na changamoto katika ukaguzi uliofanywa kwenye njia hiyo ambapo hapo awali ingelazimu kuzima umeme laini hiyo ambapo ingepelekea maeneo yanayopata umeme kupitia njia hiyo kukosa huduma kipindi cha matengenezo.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo mhandisi kutoka Kitengo cha Usafirishaji umeme Philemon Tirukaizile amesema teknolojia hiyo imeondoa kero ya kukatika umeme kwa wananchi wakati wa matengenezo.
“Bila kuwa na teknolojia hii ya kufanya matengenezo bila kuzima umeme, tungeweza kuzima njia yetu ya kusafirisha umeme kwa muda wa masaa sita. Ina maana baadhi ya wateja wetu kuanzia hapa Chalinze kuelekea Mlandizi mpaka maeneo ya Kibaha wangeweza kukosa huduma ya umeme,” amesema,” Tirukaizile.