Waafrika kuingia Burkina Faso bure kuanzia sasa

 SERIKALI ya Burkina Faso imetangaza kufuta ada za viza kwa raia wote wa nchi za Afrika, hatua inayolenga kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa ndani ya bara hilo.

Tangazo hilo lilitolewa Alhamisi baada ya kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoongozwa na kiongozi wa kijeshi, Kapteni Ibrahim Traoré. “Kuanzia sasa, raia yeyote wa Afrika anayetaka kuingia Burkina Faso hatatozwa ada ya viza,” alisema Waziri wa Usalama, Mahamadou Sana.

Kwa mujibu wa taarifa ya serikali, uamuzi huo unaashiria mshikamano wa Pan-Afrika, na pia unatarajiwa kukuza utalii, utamaduni na taswira ya Burkina Faso kimataifa. Hata hivyo, raia wa Afrika bado watalazimika kutuma maombi ya mtandaoni kabla ya kusafiri ili kupata kibali cha kuingia.

Burkina Faso, ambayo kwa sasa inakabiliwa na vitisho vya usalama kutoka kwa makundi ya waasi, inaungana na nchi kama Rwanda, Ghana na Kenya ambazo zimepunguza masharti ya viza kwa Waafrika. Kapteni Traoré alichukua madaraka kupitia mapinduzi ya mwaka 2022, lakini bado hajafanikiwa kurejesha usalama ulioahidiwa.

Hatahivyo ,wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema haijulikani iwapo hatua ya viza itasaidia kuboresha taswira ya taifa hilo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii