TLP kujenga kambi za wazee 2,000 kila mkoa

CHAMA cha Tanzania Labour (TLP) kimesema kikipata ushindi katika Uchaguzi Mkuu serikali yake itajenga kambi za kutunza wazee kwenye kila mkoa.

TLP imesema kila kambi itakuwa na uwezo wa kutunza wazee 1,000 hadi 2,000 na zitawapatia wazee mahitaji yote muhimu.

Mgombea urais kupitia chama hicho, Yustas Rwamugira amesema hayo alipohutubia wananchi kwenye mkutano wa kampeni katika Viwanja vya Tandale mkoani Dar es Salaam.

Pia, Rwamugira alisema serikali ya TLP itaanzisha vituo vya mafunzo ya vijana na shule za bweni katika kila mkoa kuwezesha vijana wa mitaani na walioacha shule wapate ujuzi wa kujitegemea.

Amesema serikali yake itabadili mtaala wa elimu kuanzia awali hadi chuo kikuu uwe wa vitendo zaidi ya nadharia.

Pia, amesema bima ya afya kwa wote na kufanya mageuzi katika sekta ya elimu ni sehemu ya ajenda yake kabambe ya kampeni zake za Uchaguzi Mkuu.

“Tutaweka mfumo ambapo nadharia na vitendo vitaenda sambamba, lakini vitendo vitakuwa na uzito zaidi ili vijana wetu wawe na tija na ubunifu,” amesema Rwamugira.

Amesema kipaumbele cha kwanza cha serikali ya TLP ni ajira na ameahidi kuchukua hatua za haraka kuwaingiza wahitimu na vijana wenye ujuzi kwenye soko la ajira.

“Ajira itakuwa jambo langu la kwanza kabisa, tuna vijana wengi, hata wahitimu wa vyuo vikuu, ambao bado hawana ajira. Tutahakikisha wanapata fursa za kufanya kazi, kujipatia kipato na kuijenga nchi yetu.” amesema Rwamugira.

Amesema rasilimali kubwa zaidi ya Tanzania ni watu wake na ardhi kubwa, ambazo zikitumika vizuri zinaweza kuchochea maendeleo jumuishi.

“Kwa kusimamia rasilimali zetu kwa ufanisi na kukusanya kodi kwa haki, Tanzania itakuwa na mapato ya kutosha kuwahudumia wananchi wake,” amefafanua.

Mgombea huyo wa TLP pia aliahidi mageuzi makubwa katika sekta ya afya. Ameahidi bima ya afya kwa wote, ikiwemo watoto, wazazi na wazee. “Kila Mtanzania atakuwa na kadi ya afya,” ametangaza.

Zaidi ya hapo, ameahidi kufuta ada za ushauri katika hospitali za serikali, pamoja na kuingiza waendeshaji wa bodaboda na bajaji kwenye mfumo wa bima kupitia benki za ngazi ya wilaya na mkoa.

Amesema mifumo hiyo itasaidia kurahisisha ukusanyaji wa mapato na kuwawezesha waendeshaji hao kupata huduma za afya.

Ameahidi kuimarisha michezo na shughuli za ziada za kielimu katika ngazi zote za masomo, huku akiahidi kuboresha viwanja vya michezo na viwanja vya kitaifa kwa ajili ya michezo mbalimbali.

Kuhusu miundombinu, Rwamugira amesema serikali yake itafufua na kuboresha Reli ya Tazara na Reli ya Kati ili zifanye kazi kwa ufanisi.

Aidha, ameahidi kazi zote za ujenzi nchini zitapewa kampuni za ndani, huku kampuni ya kigeni zikipewa nafasi za kandarasi ndogo tu.

Amesisitiza mfumo wa kodi utakuwa rafiki na wa haki kwa wananchi na taasisi zote, iwe ni za binafsi au za serikali.

Pia, aliahidi kulipa madeni yote ya ndani na nje ya nchi, huku kipaumbele kikiwa ni malimbikizo ya pensheni kwa wastaafu.

“Tunaomba amani na utulivu katika siku zote za kampeni na baada ya hapo,” amesema Rwamugira.

Makamu Mwenyekiti wa TLP Taifa, Johari Rashid alisema ni muhimu kupunguza mzigo wanaobeba akina mama katika maisha ya kila siku zikiwemo ndoo za maji kichwani na mikopo ya kausha damu.

“Lengo letu ni kuhakikisha mama anaishi kwa heshima, amani na afya njema,” amesema Rashid.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii