Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Ismail Ali Ussi amewashauri wananchi wa wilayani Kyerwa mkoani Kagera kuacha tabia ya kutunza fedha majumbani badala yake watunze benki.
Amesema kwa kufanya hivyo kutaondoa mivutano inayoweza kuhatarisha usalama na amani katika jamii na changamoto za upotevu wa fedha.
Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 umezindua Tawi la Benki ya CRDB la Nyakatuntu ambalo limegharimu Sh milioni 358 na ambapo litahudumia wananchi wa zaidi ya kata 10 za wilaya hiyo.
Kiongozi huyo amesema kuanzishwa kwa tawi hilo ni kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya sita kwani CRDB wameshawekeza katika miradi kama hiyo maeneo mbalimbali ya nchi, ambapo lengo ni kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwasogezea huduma hiyo karibu.
“Wananchi wengi wa Nyakatuntu ni wakulima,wafanyabiasha na wafugaji hivyo mnauza bidhaa na kupata fedha, nawashauri tuondokane na kutunza fedha majumbani na vikundi vya mitaani njooni benki mkafungue akaunti na kuweka fedha zenu sehemu salama,”amesema Ussi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Matawi ya Benki ya CRDB, Boneventure Paul amesema kuanzishwa kwa mradi huo ni kurahisisha upataikanaji wa huduma za kifedha,kupunguza umbali uliokuwepo katika kufuata Huduma za kifedha, kutoa ajira, kuongeza kipato kwa jamii, mapato ya serikali kupatia kodi ya serikali, ushuru wa huduma na kuongeza usalama wa utunzaji fedha kwa wananchi na serikali.
Jovini Jacob na Selestina Samsoni ni wanachi wa eneo la Mugakolongo wanasema walikuwa wakitembea umbali wa kilometa 17 kwenda kata ya Nkwenda kufuata huduma za kifedha na wakipanda pikipiki nauli ni kati ya Sh 5000 hadi 6000 kufuata huduma za benki.
Jacob amesema kujengwa kwa tawi hilo kutawasaidia kutunza fedha zao kwa usalama tofauti na walivyokuwa wakifanya nyuma kutunza fedha ndani na kisha kuibiwa au kutapeliwa na kusababisha uvunjifu wa amani kati ya ndugu ikiwemo kipigana na kuumizana.