Ripoti mpya yapendekeza hatua za haraka zichukuliwe kukabili changamoto za kujifunza

Ripoti mpya ya elimu imependekeza kuchukuliwa hatua za haraka na madhubuti za kisera zinazotokana na utafiti ili kukabiliana na tatizo la umaskini wa kujifunza duniani baada ya kubainika kuwa watoto wengi hukosa uwezo wa kusoma na kuelewa maandishi wakiwa na umri wa miaka 10.

Ripoti hiyo iliwasilishwa katika Mkutano wa Sita wa Education Evidence for Action (EE4A) na EDF, hufanyika kila baada ya miaka miwili, kabla ya kuzinduliwa rasmi baadaye mwaka huu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, msingi wa elimu hasa kusoma ni nguzo muhimu ya maendeleo ya baadaye ya mwanafunzi, huku ikionyesha mbinu shirikishi za ufundishaji, mafunzo endelevu ya walimu na uchukuaji wa hatua stahiki vina uwezo wa kuboresha matokeo kwa kiwango kikubwa.

Ripoti imeandaliwa na What Works Hub for Global Education (WWHGE) kwa ushirikiano na Shirika la Global Education Evidence Advisory Panel (GEEAP) na British Council.

Akizungumza kwenye kikao maalumu cha viongozi wa elimu, WWHGE, Profesa Kwame Akyeampong,  Mtaalam wa Elimu ya Kimataifa na Maendeleo katika Chuo Kikuu Huria, Uingereza, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha tafiti za kimataifa, ikiwemo Ripoti ya GEEAP, zinatafsiriwa katika sera na utekelezaji mashuleni ili kutoa matokeo chanya kwa wanafunzi.

Mkutano huo ulioandaliwa na Zizi Afrique Foundation uliwakutanisha wadau wa elimu na watafiti kujadili namna ya kutumia ushahidi wa kitaaluma kuimarisha sera na vitendo mashuleni.

WWHGE, ambalo linajumuisha washirika 12 wa kimkakati na 43 wa muungano na kufadhiliwa na Serikali ya Uingereza pamoja na Gates Foundation, linasaidia nchi mbalimbali kugeuza mapendekezo ya kitaaluma kuwa mageuzi ya vitendo yanayoboresha ufundishaji na ujifunzaji.

Aidha, mpango wa British Council – Learning and Life for Global Education (LL4GE) uliwasilishwa, ukionyesha namna unavyounganisha kusoma, lugha na stadi za maisha ili kuwaandaa vijana kwa ajira, ustahimilivu na uwajibikaji wa kiraia.

Kwa pamoja, WWHGE, GEEAP na British Council wameeleza kuwa ushirikiano wao ni njia ya kuhakikisha mageuzi ya elimu yanachochea matokeo endelevu na kila mtoto anafaidika na mikakati iliyothibitishwa katika kujifunza kusoma na kuandika.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii