Machar afunguliwa mashtaka Sudan Kusini

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini, Riek Machar, amefunguliwa mashtaka mazito ya mauaji, uhaini na uhalifu dhidi ya binadamu, hatua inayohofiwa inaweza kuibua upya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Waziri wa Sheria, Joseph Geng Akech, amesema mashitaka hayo yanahusiana na shambulio lililotokea Machi mwaka huu, linalodaiwa kufanywa na wanamgambo wanaohusishwa na Machar. Kwa sasa barabara zinazoelekea kwenye makazi yake mjini Juba zimefungwa, huku vifaru na wanajeshi wakipewa doria.

Machar, ambaye kwa muda mrefu amekuwa mpinzani wa Rais Salva Kiir, aliwahi kuongoza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano kabla ya makubaliano ya amani ya 2018. Ingawa makubaliano hayo yalisitisha mapigano yaliyosababisha vifo vya takriban watu 400,000, mvutano kati ya Machar na Kiir umeendelea kushika kasi.

Mbali na Machar, washirika wake saba akiwemo Waziri wa Petroli, Puot Kang Chol, na Naibu Mkuu wa Majeshi, Luteni Jenerali Gabriel Duop Lam, pia wameshtakiwa na bado wako kizuizini. Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na nchi jirani zimetoa wito wa utulivu, zikihofia hatari ya taifa hilo dogo zaidi duniani kurejea vitani.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii