Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) @airtanzania_atcl imezindua rasmi safari za moja kwa moja kutoka Dar es salaam hadi Pemba kupitia Unguja, safari hizi zinalenga kurahisisha machaguzi ya safari na kukuza utalii visiwani Zanzibar.
Akizindua safari hizo Kisiwani Pemba, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ameeleza kuwa fursa za kiuchumi, kama vile utalii na biashara, zitaimarika kisiwani Pemba kufuatiwa kurejeshwa kwa safari za ndege za ATCL.
“Kumekuwa na ndege nyingi hapa Pemba lakini sasa kwa kutumia ndege aina ya De Havilland Q400 za Air Tanzania, kutapunguza sana gharama na kuongeza machaguzi kwa wasafiri” amesema Mbarawa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mhandisi Peter Ulanga, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea.
“Uwekezaji huu umefanikisha upanuzi wa mtandao wetu wa safari za Mtwara, Iringa na Kinshasa zilizozinduliwa hivi karibuni kwa kufuatana na ambazo zote zimepokelewa vizuri sana na wadau wetu. Sasa tunatarajia kuanza safari za Lagos” amesema Ulanga.
Ulanga amebainisha kuwa kabla ya kurejesha safari za Pemba, Air Tanzania imekuwa ikifanya kwa Zanzibar safari 20 kwa siku, sawa na zaidi ya safari 140 kwa wiki.