Tanzania na Japan zaweka hati ya makubaliano sekta ya ujenzi

Tanzania na Japan zimesaini Hati ya Makubaliano ya ushirikiano (MoU) katika uendelezaji wa rasilimali watu katika sekta ya ujenzi. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Naibu Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Usafirishaji na Utalii (anayeshughulikia Miradi ya Kimataifa) wa Japan, Kenichi Ogasawara wametia saini hati hizo jijini Yokohama pembezoni mwa Mkutano wa TICAD9.

Kupitia makubaliano hayo na kwa kuzingatia teknolojia ya Japan na kampuni zake katika miundombinu bora inayodumu kwa muda mrefu na inayostahimili changamoto za mabadiliko ya tabianchi, Tanzania itanufaika kuwajengea uwezo vijana wa kada za uhandisi na ujenzi kupata teknolojia na ujuzi wa Japan ili waweze kujiajiri katika kada za ujenzi na kupata ajira katika kampuni za Japan.

Makubaliano hayo yatasaidia katika kushirikisha vijana wa Tanzania na sekta binafsi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 kupitia sekta ya miundombinu bora ambayo ni sekta mtambuka katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania.

Tanzania ni nchi ya kwanza barani Afrika kuingia makubaliano hayo na Japan katika sekta ya ujenzi, Japan imewahi kuingia makubaliano haya na baadhi ya nchi za kusini mashariki mwa Asia ambazo kupitia teknolojia bobevu ya Japan katika miundombinu bora imechagiza maendeleo ya kiuchumi ya nchi hizo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii