Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imepanga kufunga kamera maalum za usalama (CCTV) katika Daraja la J.P. Magufuli linalounganisha Kigongo na Busisi, mkoani Mwanza, ili kuhakikisha daraja hilo linalindwa ipasavyo na kudumu kwa muda mrefu kwa manufaa ya taifa.
Hayo yameelezwa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Ambrose Pascal, ambapo amesema tayari mkandarasi aliyejenga daraja hilo ameongezewa mkataba wa kutekeleza kazi ya kuweka mifumo hiyo ya usalama, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kituo cha polisi na chumba maalum cha ufuatiliaji kwa kutumia kamera.
“Kwa sasa daraja linalindwa saa 24 na askari wa usalama, lakini tumeamua kuongeza ufanisi kwa kutumia teknolojia ya kisasa kwa kufunga kamera na kujenga kituo cha ulinzi. Hii ni hatua ya kuimarisha usalama na kudhibiti vitendo vyovyote vya kihalifu, kama inavyofanyika kwenye madaraja makubwa katika mataifa yaliyoendelea,” alisema Mhandisi Pascal.
Tangu kuzinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hatareh juni 19 mwaka huu raja la J.P. Magufuli limeendelea kushuhudia ongezeko kubwa la watumiaji wakiwemo waendesha magari, bajaji na pikipiki, hivyo kuhitaji mfumo madhubuti wa uangalizi.
Mhandisi Pascal pia amewataka wananchi kulinda daraja hilo kwa kulitunza na kuepuka vitendo vya uharibifu ili liweze kutoa huduma kwa miongo kadhaa kama ilivyokusudiwa.
Aidha ametoa wito kwa vijana wa maeneo ya jirani kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi na biashara zinazochipuka kutokana na shughuli nyingi za usafiri na usafirishaji katika eneo hilo muhimu la miundombinu ya taifa.