“BONGE LA DADA” kutokea nchini Marekani , Lizzo ambaye ni “wa moto” sana katika soko la muziki wa Rap ulimwenguni, amesema kuwa kuna kipindi aliwahi kukata tamaa kabisa na kuona ni bora asiendelee kuishi duniani.
Akizungumza wakati wa mahojiano na Jarida la WOMEN’S HEALTH kutoka nchini Uingereza, rapa huyo wa kike (37) amesema kuwa hali hiyo ilimkuta mnamo mwaka 2023 baada ya kupata msongo wa mawazo kutokana na kesi kadhaa ambazo zilimuandama nje ya matarajio yake katika maisha yake.
Moja ya Kesi ambayo “ilimvuruga” akili, ni pamoja na mashtaka yaliyofunguliwa na “dansa” wake kuwa Lizzo alimfanyia unyanyasaji wa kingono kipindi wapo katika majukumu yao ya kawaida, madai ambayo Lizzo aliyakataa na kulalamika kupitia mitandao ya kijamii kuwa ni ya kipuuzi na hayana mashiko, hivyo ni vema yakapuuzwa mara moja
“Ilifikia muda nikafikiaria kwamba, kwanini nisife tu?. Sikuchukua maamuzi ya kujiua, lakini niliwaza kwamba kama mtu anafikia hatua ya kukuchukia na kukuchukulia kama wewe ni mtu muovu sana, sasa nini hatma yake?” alisema Lizzo
Hata hivyo msanii huyo aliibuka kidedea katika kesi hiyo, na hivi sasa anaishi maisha yake mazuri tu na yenye furaha bila msongo wa mawazo tena kuhusu masuala ya kesi