WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza Wizara ya Kilimo kuweka utaratibu wa kuzisaidia taasisi zinazojihusisha na kilimo zikiwemo Magereza na JKT kwa kuzipatia zana za kisasa kama mitambo ya kupandia, kuvunia na umwagiliaji kwa utaratibu wa mkopo ili kuongeza tija.
Ametoa agizo hilo Agosti 3 mwaka huu jijini Dodoma wakati akizungumza na wadau wa ushirika na wananchi waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Ushirika Kitaifa yaliyofanyika katika Kijiji cha Ushirika, ikiwa ni sehemu ya maonesho ya Nanenane ya mwaka huu.
Majaliwa amesema katika misimu miwili ya kilimo ya 2023/24 na 2024/25, pembejeo za thamani ya Sh trilioni moja zilisambazwa kwa wakulima kupitia ushirika na mazao ya Sh trilioni 6.2 yaliuzwa kupitia vyama vya ushirika.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli amesema baadhi ya vyama vya ushirika vinafanya biashara ya kimataifa na matarajio ni baadhi ya SACCOS kubadilika kuwa benki ndani ya miaka mitatu.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dk. Benson Ndiege amesema hadi sasa mali 4,990 za ushirika zenye thamani ya Sh trilioni 1 zimesajiliwa kwenye mfumo wa kidigitali na wanachama milioni 4 wamesajiliwa kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika Tanzania (MUVU).
Dk. Ndiege ameeleza kuwa mfumo wa stakabadhi za ghala umewezesha mauzo ya mazao ya Sh trilioni 4, na sasa unatumika katika mikoa zaidi ikiwemo Songwe, Shinyanga na Geita.