Mwaka mmoja baada ya Sheikh Hasina kukimbia, nchi yaandika Katiba yake mpya

Mwaka mmoja uliopita, tarehe 5 Agosti 2024, Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina alikimbia nchi, akishinikizwa na wiki kadhaa za maandamano. Wanafunzi walikuwa wakipinga mageuzi ya kujiunga na chuo kikuu na, zaidi ya yote, ukatili wa utawala wake. Tangu wakati huo, mwanauchumi na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Mohammad Yunus ameongoza serikali ya mpito. Uchaguzi unatarajiwa kufanyika mwaka ujao. Wakati huo huo, mageuzi makubwa ya kitaasisi yamezinduliwa, pamoja na rasimu ya Katiba mpya.


Kazi ni kubwa kwa serikali ya mpito. Lengo lake ni kurekebisha taasisi za Bangladesh, ambazo zimepotoshwa kwa maslahi ya kile kilichokuwa chama cha serikali: Awami league ya Waziri Mkuu wa zamani Sheikh Hasina. Hii inahitaji marekebisho ya polisi, mahakama, na tume ya uchaguzi, miongoni mwa mambo mengine. Na kazi imeanza kwa kutunga Katiba mpya.

Haya yote yamesimamisha mfumo wa kidemokrasia. Kwa mwaka mmoja, serikali ambayo haijachaguliwa ya Muhammad Yunus imekuwa ikiendesha nchi peke yake, kwani Bunge pia lilisitishwa. Uchaguzi ujao umepangwa kufanyika majira ya kuchipua mwaka ujao, lakini swali tayari linatokea: jinsi ya kujaza ombwe lililotokana na kupigwa marufuku kwa chama cha Awami League, ambacho kimetawala maisha ya kisiasa kwa miaka 15 iliyopita?

Ni chama kimoja tu kikuu, cha wanaharakati wa Kiislamu wa BNP, ndicho kilichosalia, na kinaweza kushinda uchaguzi. Isipokuwa tu chama kipya cha wanafunzi kufanikiwa kukua kujidhayiti kabla ya uchaguzi, ili kutoa mbadala mpya wa kidemokrasia nchini Bangladesh. Kwa vyovyote vile, wakati huu muhimu kwa Bangladesh pia unazua swali la mahali pa dini katika nchi yenye vyama vya Kiislamu vyenye ushawishi mkubwa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii