CHAMA cha Makandarasi na Watoa Huduma za Kikandarasi (TUCASA), kimeikumbusha serikali kuchukua hatua madhubuti kuzuia ucheleweshaji wa malipo kwa hususani kwa makandarasi wazawa wanaotekeleza miradi ya maendeleo nchini.
TUCASA imesema ucheleweshaji wa malipo sio tu unaathiri utekelezaji wa miradi bali pia inavuruga mzunguko wa fedha na kuhatarisha ustawi wa kampuni za kizalendo kushiriki kikamilifu katika ajenda ya ujenzi wa taifa.
Haya yamebainishwa na Ofisa Mahusiano TUCASA, Harris Kapiga alipozungumza na waandishi wa habari Julai 30 mwaka huu jijini Dar es Salaam kuelekea mkutano wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika Agosti 2 hadi 3 mwaka huu mkoani humo.
Kapiga amesema mkutano huo utajadili masuala mbalimbali ikiwemo kubadilishana uzoefu kuhusu mifumo kutangaza zabuni iliyowekwa na serikali kama vile NeST lakini pia kujadili changamoto mbali mbali ikiwemo ucheleweshaji wa malipo kwa makandarasi.
Kapiga amesema ucheleweshaji wa malipo umekuwa changamoto kwa makandarasi wa ndani, hali inayowalazimu baadhi yao kukopa kwenye taasisi za kifedha kwa masharti magumu, huku wengine wakishindwa kabisa kumalizia miradi kwa wakati.
“Bila hatua za makusudi kuchukuliwa, sekta ya ujenzi inaweza kudhoofika, na ajira kwa Watanzania wengi kupotea.” amesema.
Mkutano huo wenye kauli mbiu ‘Makandarasi na Watoa Huduma Wazawa ni Nguzo ya Uchumi wa Taifa’ unatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya Makandarasi na Watoa Huduma za Kikandarasi 500 nchi nzima.