GGML YATOA TAULO ZA KIKE ZAIDI YA ELFU 80 GEITA

Geita, Agosti 1, 2025 – Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imeendeleza juhudi zake za kusaidia watoto wa kike kuondokana na changamoto ya kukosa masomo wakati wa hedhi kwa kutoa taulo za kike kwa shule za msingi na sekondari zinazozunguka mgodi huo mkoani Geita, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa walimu wa malezi.

Mgodi huo umekabidhi taulo za kike takribani 80,000 kwa wanafunzi wa shule mbalimbali ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuongeza ufaulu wa wanafunzi hao na kupunguza utoro mashuleni.

Sambamba na hilo, walimu wa malezi wapatao 129 kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Geita walipatiwa mafunzo maalum ya afya ya uzazi, ili kuwajengea uwezo wa kuwahudumia kwa ufanisi zaidi wanafunzi wa kike.

Akizungumza wakati wa hafla ya mafunzo hayo, Afisa Elimu Kata ya Bugulula, Bw. Samike Deus Samike, pamoja na Kaimu Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Bi. Rehema Mustapha, walipongeza hatua hiyo ya GGML huku wakieleza kuwa imechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza utoro wa wanafunzi wa kike wakati wa hedhi na kuwafanya kuwa salama na kujiamini wakati wote.

“Zamani, kutokana na ugumu wa maisha, baadhi ya wanafunzi walikuwa hawafiki shuleni wakati wa hedhi na kukosa masomo, lakini toka GGML iwe na utaratibu huu, hali imebadilika,” amesema Bi Rehema.

Katika tukio la kugawa taulo za kike kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari Nyakabale, walimu wa shule hizo waliungana kupongeza mpango huo, ambapo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyakabale, Bi. Veronica Samo, alisema kuwa hatua hiyo imeleta mabadiliko chanya kwa mahudhurio ya wanafunzi wa kike shuleni. Naye Mwalimu wa Malezi wa Shule ya Sekondari Nyakabale, Bi. Rosemary Nichoraus, alieleza kuwa msaada huo ni muarobaini wa changamoto waliokuwa wakikumbana nazo wasichana kipindi cha hedhi.

Kwa upande wake, Afisa Uhusiano wa GGML, Bi. Doreen Denis, alisema kuwa mgodi huo umeendelea kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii zinazouzunguka mgodi huo, na kwamba hatua hiyo ni sehemu ya mpango mpana wa kampuni hiyo wa kusaidia wasichana kubaki shuleni na kufikia ndoto zao. Aliongeza kuwa zaidi ya taulo za kike 80,000 zimetengwa kwa mwaka huu kusaidia juhudi hizo.

Mpango huu wa GGML unaakisi dhamira ya kampuni hiyo katika kuunga mkono maendeleo ya elimu na ustawi wa watoto wa kike nchini Tanzania.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii