RC Simiyu aalika wananchi maonyesho ya Nanenane

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, ametoa wito kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya ziwa Mashariki na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi katika maonesho ya Nanenane yatakayofanyika kwenye viwanja vya Nyakabindi, Simiyu.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya wakuu wa mikoa ya Kanda ya ziwa Mashariki, Macha amethibitisha kuwa maandalizi ya maonesho yamekamilika na taasisi mbalimbali za serikali na binafsi zimethibitisha kushiriki.

Macha ameeleza kuwa maonyesho haya ni fursa muhimu kwa wananchi kujifunza na kuboresha shughuli zao za kiuchumi

Amesema kutakuwa na wataalamu kutoka taasisi za utafiti wa kilimo watakaotoa elimu kuhusu mbinu mpya za kilimo, matumizi sahihi ya pembejeo, na jinsi ya kudhibiti magonjwa na wadudu.

“Wataalamu pia watatoa mafunzo kuhusu usindikaji wa mazao mbalimbali kama vile mahindi, pamba, na viazi, ili kuongeza thamani na kupanua wigo wa soko.

“Maonesho haya pia yatawaunganisha wakulima na wafanyabiashara, kuwapa fursa ya kujenga mtandao wa kibiashara na kupata masoko ya uhakika kwa bidhaa zao,” amesema Macha na kuongeza:

“Maonesho haya ni fursa adhimu ya kujifunza, kuboresha shughuli za kiuchumi, na kuchangia katika pato la taifa.”

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii