Wabunge wakongwe viti maalumu CCM waachwa midomo wazi

WAJUMBE wa mikutano mikuu maalumu ya uchaguzi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mikoa wamepiga kura kuchagua wanachama walioomba nafasi ya ubunge wa viti maalumu.

Katika Mkoa wa Geita mwanamuziki Vicky Kamata ameshika nafasi ya nne kati ya wagombea wanane walioshindana kuwania nafasi mbili.

Katika uchaguzi huo uliofanyika katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Nyankumbu mjini Geita, Vicky alipata kura 186 kati ya kura za wajumbe 955 walioshiriki uchaguzi huo.

Vicky amewahi kuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Mkoa wa Geita kwa vipindi viwili kati ya mwaka 2010 hadi 2020.

Msimamizi wa uchaguzi huo ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita wakati akitangaza matokeo hayo juzi usiku alisema zilipigwa kura 955, kura nne ziliharibika na kura halali zilikuwa 951.

Mhita alisema Regina Mkenze alipata kura 831, Mbunge wa Viti Maalumu anayetetea kiti chake, Josephine Chagula alipata kura 654 na Catherine Mbumbe alipata kura 188.

Alisema Getruda Manyesha alipata kura 17, Naomi Maalim kura 14, Mwanaidi Shekue kura saba na Janeth Kasobi kura mbili.

Morogoro
Mkoani Morogoro, Lucy  Kombani aliwashinda wagombea wenzake wanane kwa kupata kura 1,314.

Msimamizi mkuu wa uchaguzi huo Mkuu wa Mkoa huo, Adam Malima alisema zilipigwa kura 1,653, kura saba ziliharibika na kura halali zilikuwa 1,646.

Malima alisema Sheila Lukuba alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 597. Lukuba aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro.

Wengine na kura kwenye mabano ni Josephine Kupuna (454), mwandishi wa habari Jane Mihanji (339), Aliyah Omar (236), Amina Karuma (153), Hajira Mwikoko (90), Dk Kulwa Kangeta (75) na Rahel Mashishanga (35).

Arusha
Mkoa wa Arusha, Martha Kivunge aliongoza kwa kura 1,004 na Chiko Issa alipata kura 775 huku Mbunge wa zamani Catherine Magige akipata kura 213. Wajumbe 1,245 walipiga kura na kura saba ziriharibika.

Msimamizi mkuu wa uchaguzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kennani Kihongosi alitangaza matokeo hayo juzi saa 5:45 usiku na kusema Asanterabi Lowassa alipata kura 196, Zaytuni kura 141, Navoi Mollel kura 95, Martha Amo kura 50 na Lillian Badi kura tisa.

Wagombea sita walikuwepo ukumbini na walikubaliana na matokeo. Magige aliondoka ukumbini baada ya kushuhudia kura zake kutotosha na mgombea Martha Amo hakuwepo kabisa ukumbini.

Dar es Salaam
Katika Mkoa wa Dar es Salaam, Janeth Mahawanga ameongoza kwa kupata kura 448, hivyo kutetea nafasi yake akifuatiwa na Amina Said aliyepata kura 421.

Wengine na kura kwenye mabano ni Janejelly Ntate (300), Dorcen Kahwa (119), Malda Juma (113), Mossy Msindo (59), Zainabu Janguo (42), Neema Kivja (21) na Georgina LukwembWe (17). Wajumbe 768 walihudhuria mkutano huo katika ukumbi wa PTA Sabasaba na zilipigwa kura 768, mbili ziliharibika na kura halali zilikuwa 766.

Mbeya
Wabunge wa sasa wa viti maalumu Mkoa wa Mbeya, Suma Fyandomo na Maryprisca Mahundi wameshinda katika kura za maoni wakiwashinda wenzao sita.

Msimamizi wa uchaguzi huo Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Simon Siro alisema Suma aliongoza kwa kura 1,152 akifuatiwa na Maryprisca aliyepata kura 1,150.

Wengine na kura zao kwenye mabano ni Ikupa Mwaifwani (200), Sara Mwangasa (189), Hobokela Mwamkina (72), Tumaini Mwakasege (45), Upendo Kalasa (18) na Anna Mwangolombe (7). Siro alisema zilipigwa kura 1,418, kura halali zikiwa 1,415 na tano ziliharibika.

Kigoma
Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Zainab Katimba ameongoza kura za maoni viti maalumu Kigoma.

Msimamizi wa uchaguzi huo Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evance Mtambi alisema Katimba aliongoza kwa kupata kura 973 kati ya kura halali 1,056.

Mtambi alisema zilipigwa kura 1,065 na kura tisa ziliharibika. Wengine na kura kwenye mabano ni Naomi Mwaipopo (686), Mwenyekiti mstaafu wa UWT Mkoa wa Kigoma, Selina Makabe (176), Ashura Kahoye (89), Amina Kaumo (80), Sabrina Sungura (71), Jackline Rugo na Prisca Mapunda walipata kura 20 kila mmoja.

Pwani
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani, Hawa Mchafu ameongoza kura za maoni ubunge viti maalumu akiwashinda wenzake saba.

Katika uchaguzi uliofanyika Kibaha, Mchafu alipata 802, Mariam Abdallah kura 645, Nancy Mutalemwa kura 449, Fatuma Uwesu (71), Irene Makongoro kura 56, Sifa Mwaruka (44), Rehema Issa kura 26 na Rehema Msemo kura saba.

Mtwara
Katika Mkoa wa Mtwara, Agnes Hokororo ameongoza kura za maoni kwa kupata kura 878 akifuatiwa na Asha Motto aliyepata kura 581 na waliwashinda wagombea wenzao saba.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa ya CCM, Juma Simba alisema zilipigwa kuwa 1,464, saba ziliharibika hivyo kura halali zilikuwa 1,457.

Simba alisema Athumini Mapalilo alipata 485, Mshihiri Athuman 438, Tunza Malapo 218, Daisy Ibrahim161, Jane Chikomo 61, Dk Rahma Hingora 60 na Sophia Malandi aliyepata kura 26.

Manyara
Mkoani Manyara, Regina Ndege na Yustina Rahhi wameongoza katika kura za maoni wakiwashinda wenzao sita. Msimamizi wa Uchaguzi, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alisema Regina alipata kura 891 na Yustina alipata kura 703.

Regina alishukuru wajumbe kwa imani kwake na akaahidi kuitumikia Manyara kwa uzalendo, uadilifu na mshikamano huku Yustina akiwashukuru wajumbe kwa kura na CCM kumlea kisiasa.

Kagera
Katika Mkoa wa Kagera, Devotha Mburarugaba na Samira Amour wameongoza katika kura za maoni ubunge viti maalumu wakiwashinda wenzao sita.

Msimamizi wa uchaguzi huo Mjumbe wa Baraza Kuu UWT Taifa, Yasmin Bachu alisema wapigakura walikuwa 1,483, kura moja iliharibika hivyo kura halali zilikuwa 1,482.

Bachu alitaja waliowania na kura kwenye mabano kuwa ni Devotha (1,308) na Samira Amour (1,250), Anitha Korongo (153), Elizabeth Ngaiza (94), Anitha Bunono (52), Anitha Nyamzinga (44), Herieth Lugaju (37) na Evastina Godian (26).

Devotha aliomba wajumbe waondoe makundi kwa kuwa uchaguzi umepita na Samira ametoa mwito kwa
wagombea ambao hawakupata ushindi wasikate tamaa.

Tanga
Katika Mkoa wa Tanga, Husna Sekiboko aliongoza kwa kura 1,637 akifuatiwa na Mwanaisha Ulenge aliyepata kura 921.

Msimamizi wa uchaguzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alisema wajumbe 1,904 walipiga kura, kura 21 ilikuwa 1,885.

Babu alitaja wagombea wengine na kura zao kwenye mabano ni Macrina Clement (25), Mboni Masimba (44), Sharifa Abebe (55), Kadodo Kombo (223), Mwantumu Zodo (772) na aliyetajwa kwa jina moja Fatuma kura 55.

Dodoma
Mkoani Dodoma, Neema Majule ameongoza kwa kura 1,524 kati ya kura halali 1,583 huku kura nane zikiharibika.

Akitangaza matokeo ya mchakato huo, msimamizi wa uchaguzi, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela alisema kura 1,591 zilipigwa katika mkutano huo.

Matokeo hayo yanaonesha Neema amefuatiwa na Jesca Mbogo aliyeshika nafasi ya pili baada ya kupata kura 1,464 huku Asia Abdallah akishika nafasi ya tatu kwa kujikusanyia kura 174.

Wengine na kura zao kwenye mabano ni Stellar Mamotto (138), Raphia Kimaro (76), Joyce Kaishozi
(12), Salama Nyundo (10), Halima Zuberi (10), Dayana Ngurumo (7) na Anna Mahendeka (6).


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii