Watatu kotini kwa mashtaka 51 ya uhalifu

Wakazi watatu wa Kyela, mkoani Mbeya wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 51, yakiwemo ya kujipatia Sh1.8 milioni kwa njia ya udanganyifu na kutumia laini za simu zisizosajiliwa kwa majina yao.

Washtakiwa hao ni Daniel Mwazyele (20), Athuman Mwakoko (21) na Obadia Mwakwenda (22), ambao walisomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Yusto Ruboroga.

Wakili wa Serikali Michael Shindai alieleza kuwa mashtaka yanayowakabili ni pamoja na Kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu (24)

Kutumia laini za simu kwa majina ya watu wengine (22), Kusambaza taarifa za uongo (3), Kutakatisha fedha (1), Kuongoza genge la uhalifu (1)

Inadaiwa kuwa kati ya Mei 10 na Juni 10, 2025, washtakiwa waliongoza genge la uhalifu na walituma jumbe fupi kwa watu mbalimbali wakiomba pesa kwa udanganyifu.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, upelelezi bado haujakamilika. Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa kesi hiyo ni ya uhujumu uchumi ambayo haijasikilizwa katika ngazi ya Mahakama hiyo.

Kesi imeahirishwa hadi Agosti 12, 2025 kwa kutajwa, huku washtakiwa wakirudishwa rumande kutokana na shtaka la utakatishaji fedha kutokuwa na dhamana kisheria.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii