Tanesco Dodoma kubaini wizi wa umeme kwa baadhi ya wateja

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia Ofisi yake ya Mkoa wa Dodoma limeanza Kampeni kabambe ya ukaguzi wa Mita za Wateja ikiwa ni sehemu ya juhudi za kudhibiti upotevu wa mapato unaosababishwa na wizi wa umeme.

Katika ukaguzi uliofanyika Agosti 11 mwaka huu eneo la Makole, jirani na Shule ya Msingi Makole jijini Dodoma, Maafisa wa TANESCO wamemkamata Mteja mmoja aliyebainika kujiunganishia umeme kiholela bila kupitia kwenye Mita ya TANESCO, hali inayosababisha hasara kwa Shirika hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TANESCO, mteja huyo alitoboa waya unaotoka kwenye nguzo na kuunganisha moja kwa moja kwenye mfumo wa nyumbani, hivyo kutumia umeme bila kupimwa wala kulipiwa.

“Mteja huyu ametumia umeme nje ya mfumo wa mita kwa lugha rahisi, alikuwa anaiba umeme,” alisema Monika Mabada, Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Dodoma.

Mabada alibainisha kuwa mara baada ya tukio hilo, TANESCO ilikata mara moja huduma ya umeme kwa mteja huyo na sasa taratibu za kisheria zinaendelea kufuatwa ikiwa ni pamoja na kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi kwa kutumia mali ya umma bila kulipia.

Mabada alieleza kuwa TANESCO imesema kampeni hii ya ukaguzi wa mita ni endelevu na inalenga kufikia wateja wote katika Mkoa wa Dodoma na kwamba kampeni hiyo ilianza rasmi mwezi Agosti na inalenga kuhakikisha kila mita inafanya kazi kwa usahihi na umeme unatumiwa kwa mujibu wa taratibu za shirika.

Aidha TANESCO imewataka wateja wote waliounganishwa kiholela au wanaotumia mbinu za wizi wa umeme kujisalimisha mapema kabla ya kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii