Al Jazeera imetangaza kuwa waandishi wake watano, ikiwa ni pamoja na mwandishi maarufu sana, waliuawa katika shambulio "la kuvizia" la Israel kwenye hema lao huko Gaza siku ya Jumapili, huku jeshi la Israel likidai kumlenga mmoja wao, ambaye ilimtaja kuwa "gaidi" kutoka vuguvugu la Hamas la Palestina.
"Mwandishi wa habari wa Al Jazeera Anas al-Sharif aliuawa pamoja na wenzake watatu katika kile kinachoonekana kuwa mashambulizi ya Israel, amesema mkurugenzi wa hospitali ya al-Shifa katika mji wa Gaza," kito hicho chenye makao yake Qatar kimeripoti.
Kulingana na Al Jazeera, "al-Sharif, 28, aliuawa siku ya Jumapili baada ya hema linalotumiwa na waandishi wa habari nje ya lango kuu la hospitali kushambliwa kwa bomu." "Mwandishi wa Al Jazeera Mohammed Qreiqeh na wapiga picha Ibrahim Zaher na Mohammed Noufal walikuwa miongoni mwa wahasiriwa," imeongeza.
Katika taarifa, kituo hicho kimeshutumu "mauaji ya waandishi wetu na vikosi vya uvamizi vya Israel, kitendo (ambacho) kiinajumuisha shambulio jipya la wazi na la makusudi dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari."
Jeshi la Israel limebanisha kwamba lilimlenga Anas al-Sharif, ambaye lilimtaja kama "gaidi" ambaye "alijifanya kama mwandishi wa habari." "Alikuwa kiongozi wa kundi la kigaidi ndani ya kundi la kigaidi la Hamas na alikuwa na jukumu la kuandaa mashambulizi ya roketi dhidi ya raia wa Israel na wanajeshi wa Israel," jeshi la Israel limesema kwenye Telegram.
Mmoja wa watu mashuhuri katika uandishi wa habari akiripoti juu ya vita huko Gaza
Anas al-Sharif alikuwa mmoja wa watu maarufu sana miongoni mwa waandishi wa habari wanaoripoti vita vya Gaza kila siku. Jeshi la Israel limebainisha kuwa lilimlenga: "Alikuwa kiongozi wa kundi la kigaidi ndani ya kundi la kigaidi la Hamas na alikuwa na jukumu la kuandaa mashambulizi ya roketi dhidi ya raia na wanajeshi wa Israel," IDF imesema kwenye Telegram.
Israel iliamua mwezi Mei 2024 kupiga marufuku matangazo ya idhaa hiyo nchini humo na kufunga ofisi zake, matokeo ya mzozo wa muda mrefu kati ya chombo hiki cha habari na serikali ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ambao umeongezeka wakati wa vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza.
Jeshi la Israel limewashutumu mara kwa mara waandishi wa habari wa Al Jazeera kuwa ni "maafisa wa kigaidi" huko Gaza wenye mafungamano na Hamas, vuguvugu la Kiislamu lililohusika na shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa mnamo Oktoba 7, 2023, nchini Israel ambalo lilianzisha vita.
Takriban waandishi wa habari 200 wameuawa na jeshi la Israel
Tangu kuanza kwa vita dhidi ya Hamas huko Gaza, vyombo vya habari vya kimataifa havijaruhusiwa kufanya kazi kwa uhuru katika ardhi ya Palestina. Ni vyombo vichache tu vya habari vilivyochaguliwa kwa uangalifu ambavyo vimeingia katika eneo lililowekwa na jeshi la Israeli, kwa kurusha habari zilizo chini ya udhibiti mkali wa kijeshi. Siku ya Jumapili Benjamin Netanyahu alisema kwamba ameliagiza jeshi kuruhusu waandishi wa habari zaidi wa kimataifa kufanya kazi chini ya udhibiti wake katika Ukanda wa Gaza.
Vyombo vya habari vya kimataifa vinategemea waandishi wa habari wa ndani na maripota, ambao wamepata hasara kubwa katika mzozo huo: karibu waandishi wa habari 200 wameuawa katika kipindi cha miezi 20 na jeshi la Israeli, angalau 45 kati yao wakiuawa wakiwa katika kazi zao, kulingana na Shirika la Waandishi Wasio na Mipaka (RSF).