Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimeidhinisha rasmi ilani yake ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Uamuzi huo umetangazwa leo, Alhamisi Agosti 7 mwaka huu katika Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Akiongoza zoezi la upigaji kura za vidole kupitisha Ilani hiyo, Katibu Mkuu wa Chaumma, Salum Mwalimu amesema wanachama na viongozi wa chama hicho wako tayari kutekeleza ahadi zote zitakazotolewa kwa wananchi iwapo watapewa ridhaa ya kuongoza nchi baada ya uchaguzi huo.
“Wanaosema wako tayari kwenda kuzipigania na kuzitekeleza ahadi hii tutazopewa ridhaa na Watanzania, naomba tunyooshe mkono… Wanaosema watazisimamia pale tutakapopewa imani na Watanzania baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu nyoosha mkono,” amesema Mwalimu mbele ya wajumbe wa mkutano huo.
Baada ya wajumbe wote kuonyesha kuunga mkono, Mwalimu amehitimisha kwa kutamka kuwa: “Wote tumekubali. Mungu awabariki sana. Kwa niaba ya Mkutano Mkuu, natamka kuwa hii ndiyo Ilani ya Chama cha Ukombozi wa Umma,”.