Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Benson Kigaila amemtangaza Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu atakuwa mpeperusha bendera wa chama hicho kwenye mbio za urais wa Tanzania Oktoba 29 mwaka huu.
Kigaila amemtangaza kiongozi huyo kwenye mkutano mkuu wa Chaumma unaoendelea Mlimani City leo Alhamisi Agosti 7, 2025.
Kigaila amesema jina la kiongozi huyo lilipendekezwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho yenye jukumu la kuleta mapendekezo ya jina la mgombea urais Tanzania na Zanzibar katika kikao kilichofanyika jana.
"Baada ya kufanya utafiti na kufikiri kwa kina ni mtu gani anaweza kutuvusha, Halmashauri Kuu ya Taifa ilikuja na jina la Salum Mwalimu, anatufaa kutuvusha kwenye mbio za urais wa Tanzania," amesema Kigaila.
Kulingana na maelezo ya Kigaila amesema mchakato wa kumpata Salum waliopitia hadi kufika kupata, kwanza walifanya utafiti na katika kutafiti huu:"Tuliangalia nani anaweza kutufaa na kutuvusha, tulifanya mazingatio tukimteua mtu anajua matatizo ya Watanzania akiona anaweza kuumizwa na kuyashughulikia."
Vile vile mgombea urais wa Chama hicho Salum Mwalimu ametangaza rasmi kumteua, Devotha Minja kuwa mgombea mwenza wake katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Aidha ameeleza kuwa uteuzi huo wa Minja ni sehemu ya dhamira ya Chaumma kuwaleta pamoja viongozi wenye maono na rekodi ya kupigania haki za wananchi, ili kuleta mabadiliko ya kweli nchini.
Hata hivyo Devotha ni mwanasiasa aliyewahi kushika nafasi mbalimbali ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ikiwa ni pamoja na kuwa mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Kati.