Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo Dorothy Semu amedai kuwa wa chama hicho kiko vitani si kwa silaha bali ni kwa ajili ya kurejesha heshima ya kura na kulinda demokrasia ya kweli nchini.
Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa chama hicho Dorothy amesema kuwa ACT-Wazalendo haikuchaguliwa kushiriki uchaguzi kwa mapenzi, bali kwa dhamira ya kulinda haki za wananchi na kuchagua viongozi wao huku akisisitiza kuwa ushiriki wao ni hatua ya kishujaa dhidi ya mfumo dhalimu wa kisiasa.
“Tulipokutana Halmashauri Kuu mwezi Februari mwaka huu niliwaeleza kuwa chama chenu kinatambua kuwa CCM wanajua hawawezi kushinda uchaguzi wa haki. Wanajua wananchi hawawataki. Ndiyo maana wanajificha nyuma ya dola, Tume, Polisi, vitisho na matumizi ya mabavu.”
Ameeleza kuwa chama kimejipanga sawasawa kudhibiti hujuma zote za kisiasa kutoka kwa dola na kuhakikisha kuwa mapambano ya kidemokrasia yanafanikiwa kwa vitendo akifananisha hali ya sasa na vita halisi ambayo inahitaji ujasiri, mkakati na mshikamano.
“Chama chetu kinapaswa kujipanga vizuri kuhakikisha tunadhibiti hujuma za CCM na dola, na kufanikisha malengo yetu ya kisiasa kama ambavyo majemedari wa vita waliweza kuusoma mwelekeo wa vita, kufufua ari ya mapambano, na kusonga mbele hadi kuupata ushindi,” aliongeza.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo ameleza kuwa jambo la kususia uchaguzi halikuwahi kuleta mabadiliko ya kweli hivyo ACT-Wazalendo imeamua kupambana ndani ya uwanja wa kisiasa kwa dhati hadi haki itendeke.
“Mapambano ya kweli ni ya wale wanaojitosa uwanjani. Na sisi, ACT Wazalendo, tumeingia vitani na tutatoka na ushindi,” alisema.