Serikali kupitia Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), imesema kuwa imeendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi na uagizaji mafuta nchini kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi, salama na ya uhakika kwa wananchi wakati wote.
Akizungumza leo Agosti 7 mwaka huu katika mkutano na Wahariri pamoja na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa PBPA, Erasto Simon, amesema Serikali imeweka kipaumbele katika utekelezaji wa sera ya nishati inayolenga kuhakikisha Watanzania wanapata nishati bora kwa gharama stahiki.
“Lengo la Serikali kuanzisha taasisi kama PBPA ni kutekeleza sera ya nishati ambayo inalenga kuhakikisha nchi inapata nishati safi, salama na ya uhakika wakati wote. "Ili kufanikisha hili, lazima tuhakikishe pia kuna usalama wa utunzaji wa mafuta katika maeneo yote nchini,” alisema Simon.
Ameeleza kuwa kwa kushirikiana na wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), na taasisi kama EWURA, Serikali imefanikiwa kuboresha mifumo ya kifedha ili kuwawezesha wafanyabiashara wa mafuta kulipia kwa wakati kupitia mfumo wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja (BPS).
Aidha amesema, Serikali imefanya maboresho katika mikataba ya uletaji wa mafuta ili kuwapa fursa wafanyabiashara kutumia njia mbadala za malipo badala ya kutegemea Dola pekee, hatua inayolenga kuongeza unafuu na ufanisi katika upatikanaji wa mafuta nchini.