SERIKALI ya Uingereza imetangaza mikakati mipya ya kudhibiti upasuaji wa kuboresha mwonekano wa mwili, ikiwemo kuongeza makalio, kukuza midomo, pamoja na kuondoa mikunjo usoni, kwa lengo la kuwalinda watu hasa walio chini ya umri wa miaka 18.
Taarifa hiyo imetolewa kufuatia ongezeko la wasiwasi kuhusu upasuaji huo kufanyika katika mazingira yasiyo salama kama majumbani, kwenye mahoteli au katika kliniki za muda ambazo hazijasajiliwa, hali inayohatarisha maisha ya wagonjwa.
Kwa mujibu wa mpango huo, serikali imesisitiza kuwa ni madaktari waliobobea katika tiba ya urekebishaji wa maumbile (cosmetic surgery) pekee ndio watakaoruhusiwa kufanya upasuaji huo, huku wateja wadogo wa chini ya miaka 18 wakizuiwa kabisa kupata huduma hizo.
Hatua hiyo inalenga kulinda afya na usalama wa wananchi, hasa vijana, katika kipindi ambacho matumizi ya mitandao ya kijamii na shinikizo la kijamii vimetajwa kuchangia ongezeko la watu wanaotaka kubadilisha muonekano wao kwa njia za upasuaji.