Uingereza imekuwa nchi ya kwanza duniani kuanza kutoa chanjo dhidi ya maambukizi ya gonorrhea, ikiwa ni hatua muhimu katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo wa zinaa ambao umekuwa ukiongezeka kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni.
Chanjo hiyo mpya inalenga makundi yaliyo katika hatari kubwa ya maambukizi, hasa wanaume wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja pamoja na watu wenye historia ya kuwa na wapenzi wengi.
Lengo kuu ni kuwalinda watu walio katika mazingira ya hatari zaidi huku ikiisaidia jamii kwa ujumla kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo.
Gonorrhea huambukizwa kwa njia ya kujamiiana, unasababishwa na bakteria aitwaye Neisseria gonorrhoeae. Ugonjwa huu unaweza kuathiri sehemu mbalimbali za mwili kama vile sehemu za siri, rektamu, koo na hata macho.
Ikiwa hautatibiwa mapema, unaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya ikiwemo ugumba, maambukizi ya damu na maumivu ya kudumu ya nyonga kwa wanawake.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Idara ya Afya ya Umma ya Uingereza (UKHSA), maambukizi ya gonorrhoea yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 50 katika kipindi cha miaka michache iliyopita, hali inayotia hofu na kuhitaji hatua madhubuti.
Chanjo hii mpya inajulikana kama 4CMenB, ambayo hapo awali ilikuwa ikitumika kwa ajili ya kuzuia meningitis B, lakini tafiti zimeonyesha kuwa ina uwezo pia wa kutoa kinga dhidi ya gonorrhoea kwa zaidi ya asilimia 30 hadi 40. Ufanisi huo, ingawa si wa kiwango cha juu kabisa, ni hatua ya mwanzo muhimu katika kudhibiti ugonjwa huo sugu.
Wataalam wa afya wanahimiza watu walio katika makundi lengwa kujitokeza kwa hiari kupokea chanjo hiyo na pia kuendelea kujikinga kwa kutumia kondomu na kufanya vipimo vya mara kwa mara.