Chama cha siasa cha NRA yaja na ilani inayozingatia huduma kwa wananchi

Mustakabali wa kisiasa wa Tanzania unapata matumaini mapya kupitia Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA) ambacho kimezindua ilani yake kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa kuweka mbele masilahi ya taifa badala ya vyama vya siasa.

Kikiwa na kaulimbiu yake ya “Taifa Kwanza, Vyama Baadaye”, chama hicho kieleza maono yake yanajieleleza kwenye huduma za afya na elimu bure, ulinzi wa kijamii kwa wote, serikali ya umoja wa kitaifa, kufufua mchakato wa mabadiliko ya Katiba, na mageuzi katika kilimo, viwanda, teknolojia na ajira.

Katika ilani yake ya mwaka 2025–2030, chama hicho kimewasilisha mpango kabambe wa kujenga upya imani ya wananchi kwa Serikali, kufufua huduma muhimu na kurejesha utawala unaoongozwa na wananchi.

Moja ya mapendekezo makuu ya chama hicho ni kuunda serikali shirikishi itakayojumuisha watu kutoka pande zote za kisiasa, bila kujali itikadi ya vyama.

Mgombea urais wa chama hicho, Hassan Almas amesema NRA haioni uongozi wa vyama kama suluhisho. Badala yake, inaamini katika uongozi unaokumbatia utofauti wa mawazo na uzoefu.

“Tutaunda Serikali inayoheshimu vyama vyote vya siasa, mikoa yote, dini zote na makabila yote. Hii italeta umoja wa kitaifa,” amesema Almas katika hotuba yake kwa umma.

Ahadi kubwa ya NRA ni kutoa huduma muhimu bure kwa wananchi wote. Ilani hiyo inaahidi elimu bure kuanzia chekechea hadi sekondari ya juu, ikiwa ni pamoja na kutoa vifaa vya kujifunzia na usafiri wa wanafunzi.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii