Zaidi ya wakulima 18,000 watarajia kunufaika na Kilimomisitu

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kuwa zaidi ya wakulima 18,000 wanatarajiwa kunufaika moja kwa moja na Mpango wa Taifa wa Kilimomisitu ifikapo mwaka 2031, ambao unalenga kuhakikisha wakulima milioni 15 wanatumia teknolojia na mbinu bora za kilimomisitu nchini.

Mkakati huo uliozinduliwa mwaka 2024 na Mhe Dkt. Philipo Isdori Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umejikita katika kuendeleza kilimomisitu nchini, ikiwa na dhima ya kukuza ufanisi wa mbinu za kilimomisitu na teknolojia zake ili ziweze kutumika na jamii ya wakulima kwa ajili ya kudumisha ustawi wa jamii, uchumi na mazingira.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Kitaifa ya Ushauri ya Kilimomisitu, Waziri Chana alisema kuwa Mkakati huo uliopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii na unalenga kukuza ufanisi wa matumizi ya teknolojia za kilimomisitu ili ziweze kutumiwa na jamii ya wakulima katika kuboresha ustawi wa jamii, uchumi na mazingira.

“Ili kuhakikisha utekelezaji wa mkakati huu unafanyika kwa ufanisi, Wizara imeunda Kamati ya Kitaifa ya Ushauri ambayo leo naizindua rasmi. Kamati hii itakuwa na jukumu la kushauri na kusimamia utekelezaji wa mkakati huu,” amesema Waziri Chana.

Alifafanua kuwa Tanzania ina jumla ya hekta milioni 48.1 za misitu, sawa na asilimia 55 ya eneo la nchi kavu, ambapo asilimia 93 ni misitu ya uoto wa Miombo na asilimia 7 ni misitu ya Uwanda wa Chini, Milimani, Mikoko na mashamba ya miti.

Hata hivyo, alionya kuwa misitu inakabiliwa na changamoto kubwa kama uvamizi, uchomaji mkaa, moto wa misituni na uchimbaji haramu wa madini. “Takwimu zinaonesha kuwa hekta 469,400 za misitu hupotea kila mwaka. Kiwango hiki ni kikubwa mno na kinapaswa kudhibitiwa,” alisisitiza.

Alibainisha kuwa wakulima ni wadau muhimu katika utekelezaji wa Mkakati wa Kilimomisitu kutokana na nafasi yao katika kilimo na uhifadhi wa mazingira, hivyo wataunganishwa katika minyororo ya thamani ya bidhaa za kilimomisitu ili kuongeza kipato na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii