Mawaziri wawili wauawa ajali ya helikopta

WAZIRI wa Ulinzi wa Ghana, Edward Mane Boamah, na Waziri wa Mazingira, Sayansi na Teknolojia, Ibrahim Murtala Muhammed, wamefariki dunia katika ajali ya helikopta iliyotokea jana, Jumatano.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais wa Ghana, John Mahama, mawaziri hao walikuwa miongoni mwa abiria waliokuwa wakisafiri kwa helikopta ya Jeshi la Anga la Ghana iliyoanguka katika msitu ulioko kusini mwa nchi hiyo. Helikopta hiyo ilikuwa imewabeba watu wanane, wakiwemo wafanyakazi watatu wa jeshi na abiria watano.

Kituo cha televisheni cha Joy News kilirusha mkanda wa video uliorekodiwa kwa simu ya mkononi ukionesha mabaki ya helikopta hiyo yakiwa yameungua huku moshi mzito ukifuka kutoka eneo la ajali kabla ya kuthibitishwa kwamba mawaziri hao walikuwa miongoni mwa waliopoteza maisha.

Edward Mane Boamah aliteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi mapema mwaka huu, mara baada ya Rais Mahama kuapishwa rasmi mwezi Januari

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii