RAIS wa Kenya William Ruto amekemea vikali serikali ya Amerika kufuatia mpango wake wa kuchunguza uhusiano wa Kenya na China, akisisitiza kuwa ushirikiano wa kibiashara na taifa hilo la Asia ni kwa maslahi ya kitaifa ya Kenya.
Rais Ruto alisema kwamba Kenya haipaswi kulaumiwa kwa kutafuta masoko mapya ya bidhaa zake, washirika wapya wa biashara na rasilmali, hasa katika ulimwengu unaoshuhudia mvutano wa kijiografia kati ya Amerika na China.
“Baadhi ya marafiki wetu wanalalamika kwamba tunafanya biashara nyingi na China. Lakini hiyo ni lazima nifanye kwa ajili ya Kenya,” alisema Ruto.
“Tumekamilisha mazungumzo ya ngazi ya juu na China. Wamekubali kuondoa ushuru wote kwa chai yetu, kahawa, parachichi na bidhaa nyingine za kilimo. Hii ni hatua kubwa kwa taifa letu.”
Kauli ya Rais Ruto inajiri baada ya Seneta Jim Risch, mwenyekiti wa Kamati ya Mahusiano ya Kigeni ya Seneti ya Amerika, kuwasilisha mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Ulinzi ya Taifa ya mwaka wa fedha wa 2026, akitaka uhusiano wa Kenya na China uchunguzwe,
Rais Ruto alitetea msimamo wake kuhusu China, akisema alipokutana na Rais Xi Jinping, aliibua suala la usawa wa kibiashara kwani Kenya huagiza bidhaa za thamani ya Sh600 bilioni kutoka China, huku ikiuzia China bidhaa za chini ya asilimia tano ya thamani hiyo.
“Hali hiyo ya biashara si sawa, na ndio maana China imefungua soko lake kwa bidhaa zetu za kilimo. Hii ni kwa faida ya Kenya, na ni jambo la busara,” alieleza Rais.
Seneta Risch amependekeza kufutiliwa mbali kwa hadhi ya Kenya kama mshirika mkuu asiye mwanachama wa Nato (MNNA), akisema Kenya imeonyesha ‘ushirikiano wa karibu mno na China’ kiasi cha kuonekana kuwa imeapa utii kwa Beijing.
Alinukuu hotuba ya Rais Ruto aliyotoa katika Chuo Kikuu cha Peking, Beijing mnamo Aprili 23, 2025, ambapo Ruto alitaja Kenya na China kama ‘washirika katika kujenga mfumo mpya wa dunia.’
Pia, mswada huo unapendekeza kuchunguzwa kwa matumizi ya msaada wa kiusalama kutoka Amerika kwa Kenya, hasa ikiwa msaada huo umetumika vibaya kwa utekaji nyara, kutesa raia, kuwatimua kwa lazima, mauaji ya kiholela, na vitendo vya kikatili vinavyodaiwa kufanywa na polisi au vikosi vya usalama.
Kenya pia imelaumiwa kufuatia utekaji nyara wa raia saba wa Uturuki mjini Nairobi na maafisa wa kijasusi kutoka nchi hiyo mnamo Oktoba 2024.
Aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, na chama cha DAP-K wamekosoa vikali Rais Ruto wakisema hatua hiyo ya Amerika ni fedheha ya kimataifa kwa Kenya.
Gachagua alisema Kenya imegeuka kuwa kimbilio la kulangua fedha kwa washukiwa wa ugaidi na ufisadi, akiongeza kuwa serikali imeshindwa kukabiliana na makundi ya kigaidi kama Al-Shabaab na RSF ya Sudan.
“Rais Ruto tulikuonya kuhusu RSF na Al-Shabaab, tukakwambia wazuie magaidi wa kimataifa na wahalifu wa kifedha kuingia nchini. Lakini ulikataa,” alisema Gachagua.
“Hatutakubali nchi yetu itumbukie katika udikteta, ghasia na kuporomoka kwa demokrasia. Uhusiano wetu wa kiusalama na Amerika unaweza kusambaratika kabisa.”
Naye aliyekuwa waziri w Ulinzi Eugene Wamalwa alisema mjadala unaoendelea Amerika kuhusu Kenya ni ushahidi wa kushindwa kwa uongozi wa Ruto na kwamba taifa linapaswa kuepuka kumpa muhula wa pili mwaka 2027.
Katibu wa Wizara ya Masuala ya Kigeni Korir Sing’oei alijibu kupitia mtandao wa X akisema “masuala haya yaliyopo katika mswada Amerika yatajibiwa kwa kina, tukizingatia uhuru wa Kenya na maslahi ya taifa.”