Kila mwaka Serikali hutenga zaidi ya shilingi bilioni 277 kwa ajili ya kugharamia huduma mbalimbali za Virusi Vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI nchini, ikiwa ni hatua ya kupunguza utegemezi wa wafadhili wa kimataifa katika mapambano dhidi ya janga hilo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dkt. Samwel Sumba, amesema hayo katika Maonesho ya 32 ya Nanenane yanayofanyika katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma alipotembelea banda la Ofisi TACAIDS.
Dkt. Sumba amesema kuwa uwekezaji huo mkubwa wa Serikali unaonesha dhamira ya dhati ya kuimarisha afua za VVU na UKIMWI kwa kutumia rasilimali za ndani, hatua ambayo inalenga kudhibiti kwa ufanisi zaidi maambukizi mapya na kuboresha maisha ya watu wanaoishi na virusi hivyo.
“Ni muhimu kwa nchi kuanza kujitegemea kifedha katika mapambano haya, hii itasaidia kuhakikisha huduma zinaendelea kupatikana kwa uhakika na kwa wakati, hata kama misaada kutoka kwa wafadhili itapungua au kusimama,” amesema Dkt. Sumba.
Amefafanua kuwa kwa mujibu wa ripoti ya Utafiti wa Athari za UKIMWI ya mwaka 2022/2023, Tanzania inakadiriwa kuwa na watu wanaoishi na VVU kati ya 1,540,000 hadi 1,700,000 huku Kiwango cha maambukizi kwa watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi kimefikia asilimia 4.4, ambapo wanawake wanaongoza kwa asilimia 5.6 ikilinganishwa na wanaume wenye asilimia 3.0.
Hata hivyo Dkt. Sumba ameongeza kuwa pamoja na takwimu hizo, bado kuna mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha zaidi ya miaka ishirini iliyopita.