Othman Masoud mgombea pekee urais kutokae ACT Wazalendo Zanzibar

Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha ACT Wazalendo katika kikao chake maalum kilichofanyika  Agosti 5 mwaka huu katika ukumbi wa Hakainde Hichilema, imempendekeza rasmi Ndugu Othman Masoud Othman kuwa mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia tiketi ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Ndugu Othman Masoud Othman, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Taifa wa @actwazalendo_official na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ndiye mwanachama pekee aliyewasilisha fomu ya kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar ndani ya muda uliopangwa na chama. Hali hiyo imemfanya kuwa mgombea pekee kupendekezwa na Halmashauri Kuu.

Kwa mujibu wa taratibu za chama, jina lake sasa litasubiri kuthibitishwa na Mkutano Mkuu wa Taifa, chombo cha juu cha maamuzi ya chama, ambacho kitafanya uchaguzi wa mwisho wa kumpitisha mgombea rasmi.

Ndugu Othman Masoud ni kiongozi mwenye uzoefu mkubwa katika masuala ya kisheria, utawala, na siasa za Zanzibar na Muungano kwa ujumla. Kabla ya kushika nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar mwaka 2021, Othman alikuwa Mshauri Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (Attorney General), ambapo alitumikia kwa uadilifu hadi alipojiunga na ACT Wazalendo na kuibuka kuwa mmoja wa viongozi wake wakuu.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii