NEMC, Wiomsa wajadili mchango wa vyakula vya baharini, mitoni

 Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Taasisi ya WIOMSA (West Indian Ocean Marine Science Association) wameanza warsha ya siku mbili kwa wadau kutoka sekta za serikali, binafsi na kijamii ili kujadili mchango wa vyakula vya baharini, mitoni na maziwa—maarufu kama “blue foods”—katika lishe bora na usalama wa chakula.

Warsha hiyo inafanyika katika Ukumbi wa Tanga Resort, mkoani Tanga.

Akifungua rasmi warsha hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Zahor Kassim Mohamed, amesema vyakula vya buluu kama samaki, dagaa, kaa, majongoo wa baharini na mwani vina mchango mkubwa katika kuimarisha lishe, kuongeza kipato cha kaya, kuleta ajira na kulinda mazingira ya majini.

“Ni muhimu sekta zote—binafsi, serikali na mashirika ya maendeleo—kuhakikisha vyakula vya buluu vinachangia kwa ufanisi kutokomeza njaa, kuongeza ajira na kulinda mazingira ya mito, maziwa na bahari,” alisema Zahor.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Immaculate Sware Semesi, alisema warsha hiyo inalenga kuhamasisha uelewa wa kijamii kuhusu faida za vyakula vya buluu katika kujenga afya bora na jamii zenye uwezo wa kujitegemea kiuchumi.

Mkurugenzi wa WIOMSA, Dk. Arthur Tuda, akiwasilisha mada alisema taasisi hiyo imejikita kwenye tafiti na elimu kwa jamii kuhusu vyakula vya baharini, na inalenga kukuza matumizi ya chakula chenye virutubisho bora ili kusaidia mabadiliko ya mifumo ya chakula duniani.

Warsha hiyo imeelezwa kuwa sehemu ya jitihada za pamoja katika kuchochea maendeleo ya uchumi wa buluu, kuongeza thamani ya mazao ya maji na kuimarisha mnyororo wa thamani unaowashirikisha wanawake na vijana.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii