Jaji wa Mahakama ya Juu ya Brazili amewapa mawakili wa Jair Bolsonaro saa 24 kueleza "kutofuata" kwao marufuku ya rais huyo wa zamani kutumia mitandao ya kijamii, "chini ya adhabu ya kifungo cha mara moja," kulingana na hati ya mahakama.
Kiongozi huyo wa zamani wa siasa kali za mrengo wa kulia, anayekabiliwa na kesi ya jaribio la mapinduzi dhidi ya rais wa sasa wa mrengo wa kushoto, Luiz Inacio Lula da Silva, aliagizwa siku ya Ijumaa avae bangili ya kielektroniki na kuacha kutumia mitandao ya kijamii. Alitoa taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Jumatatu, ambazo zilisambazwa haraka kwenye mitandao ya kijamii ya wanawe na washirika wake wa kisiasa, na hivyo kusababisha onyo la mahakama.
Jaji amemshutumu Jair Bolsonaro, 70, kwa "kutoa hotuba iliyokusudiwa kutangazwa kwenye majukwaa ya kidijitali."
Katika kesi ya mapinduzi dhidi ya Lula, kiongozi huyo wa zamani wa siasa kali za mrengo wa kulia analazimika kuvaa bangili ya kielektroniki na kuzingatia hatua nyingine za tahadhari, kama vile kutotumia mitandao ya kijamii, kutokana na uchunguzi wa tuhuma za kuzuia utoaji haki.
Jaji wa Mahakama ya Juu Alexandre de Moraes alihalalisha hatua hizi kwa kumshutumu kwa kuchochea, pamoja na mtoto wake Eduardo, "vitendo vya uadui" vya Marekani dhidi ya Brazili na kujaribu "kuzuia" kesi, ambayo anaisimamia. Kwa kujibu, rais huyo wa zamani alitoa taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Jumatatu, ambazo zilisambazwa haraka kwenye mitandao ya kijamii, na kusababisha onyo hilo la mahakama.
Katika ofisi yake, Alexandre de Moraes kisha alionyesha machapisho kutoka kwa akaunti za X, Instagram, na Facebook na video, picha, na maandishi ya taarifa za Jair Bolsonaro kwa waandishi wa habari katika Bunge la Congress. Rais huyo wa zamani hakuchapisha hotuba hiyo kwa akaunti yake mwenyewe, lakini wanawe na washirika wake wa kisiasa walichapisha.
Alexandre de Moraes pia amewataka mawakili wa rais huyo wa zamani kutoa ufafanuzi ndani ya saa 24 "juu ya kushindwa kuzingatia hatua za tahadhari zilizowekwa, chini ya adhabu ya kuamuru kufungwa kwake mara moja."
Katika uamuzi wa hapo awali wa Jumatatu, Alexandre de Moraes ameonya kwamba matangazo yoyote ya hotuba za umma za Jair Bolsonaro kwenye majukwaa yatajumuisha ukiukaji wa hatua zinazotumika na kwamba rais wa zamani anaweza kukamatwa.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa vyama vya mrengo wa kulia na mrengo wa kulia wenye siasa kali nchini Brazili, amekashifu kile anachokichukulia kuwa ni kitendo cha "uoga" dhidi yake. "Ni ishara ya unyonge," ametangaza, akionyesha kwa mara ya kwanza bangili ya kielektroniki ambayo analazimishwa kuvaa kwenye kifundo cha mguu wake wa kushoto. "Kilicho halali kwangu ni sheria ya Mungu," ameongeza katika taarifa ambazo zilisambaa haraka kwenye mitandao ya kijamii.