TMA yataja mikoa 20 kupata mvua nyepesi na upepo mkali kwa siku 10

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetaja mikoa zaidi ya 20 ikiwemo visiwa vya Unguja na Pemba itakayokuwa na hali ya ukavu na baadhi kupata mvua nyepesi na upepo mkali kwa siku 10 kuanzia leo Jumatatu Julai 21, 2025.

Mikoa iliyotajwa kushuhudia hali ya ukavu kwa siku 10 (Julai 21-30) kwa Kanda ya Ziwa Victoria ni Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza na Mara.

“Kwa nyanda za juu kaskazini-mashariki, mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, hali ya ukavu kwa ujumla inatarajiwa,” imeeleza taarifa ya TMA kuhusu mwelekeo wa mvua kwa siku 10.

Mikoa ya Pwani ya kaskazini inayojumuisha Tanga, maeneo ya kaskazini mwa Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na visiwa vya Unguja na Pemba kunatarajiwa vipindi vya mvua nyepesi na upepo mkali maeneo machache.

Pia maeneo mengine ni magharibi mwa Tanzania ambapo TMA imeeleza mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora hali ya ukavu inatarajiwa.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii