Uchaguzi wa Madiwani wa Viti Maalum kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kwa Morogoro Mjini limehitimishwa kwa amani, huku baadhi ya vigogo maarufu wakianguka na madiwani sita wa zamani wakirejea katika nafasi hizo.
Uchaguzi huo ambao ulianza Julai 20, 2025 kwa zoezi la kupiga kura na kukesha kuhesabu matokeo hadi alfajiri ya siku ya pili, Julai 21, ulimalizika kwa kutangazwa kwa matokeo majina ya saa 12:15 asubuhi.
Idadi ya wagombea 31 ambao majina yao yalipitishwa kugombea nafasi hiyo na idadi ya kura walizopata yametangazwa na msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni Katibu wa UVCCM Morogoro mjini, Khalid King kwa kuanza na aliyepata kura ndogo hadi aliyepata kura nyingi.
Kwa utaratibu wa CCM, washindi hawatajwi moja kwa moja, bali hutangazwa majina yote ya wagombea na kura walizopata. Katika zoezi hilo ambapo vikao vikiridhia wateuliwa 10 walioongoza ama vinginevyo ndio hupitishwa kugombea.
Mwandishi wa habari wa Uhuru na Mzalendo, Latifa Said Ganzel, aliibuka kinara kwa kupata kura 934.
Waliofuata ni Batuli Kifea (794), Grace Mkumbae (752), Salma Mbandu (698), Imakulata Mhagama (581), Warda Bazia (562), Rahma Maumba (560), Magreth Ndewe (556), Anna Kisimbo (535), na Amina Zihuye (532).
Miongoni mwao, madiwani sita waliokuwa kwenye nafasi hiyo awali wamerejea, akiwemo Latifa, Grace, Salma, Warda, Rahma, na Amina.
Viongozi maarufu waliokuwa wakitetea nafasi zao, akiwemo Hadija Kibati maarufu kama ‘Mama Nyau’, Zamoyoni Abdallah na Mwanaidi Ngulungu wameanguka kwenye kinyang’anyiro hicho.