Kaburi lafukuliwa huku kichwa cha marehemu kukatwa

Jeshi la polisi Mkoani Tanga, linafanya uchunguzi na kuwasaka watu waliohusika katika tukio la kufukua kaburi na kuondoka na kichwa cha marehemu aliyezikwa na kuondoka nacho 

Kamanda wa polisi mkoani Tanga, Alimachius Mchunguzi akiwa ofisini kwake alisema jeshi hilo linafanyia uchunguzi kuhusu taarifa za watu kufukua kaburi na kundoka na kichwa na kubakisha mwili kwenye kaburi. 

Ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea Julai 18 mwaka huu majira ya saa nne asubuhi baada ya wananchi kutoa taarifa za kufukuliwa kaburi la mtu mmoja aliyezikwa katika makaburi ya familia Julai 12 mwaka huu katika Kijiji cha Mgela kilichopo wilayani Kilindi. 

Kamanda Mchunguzi alimtaja marehemu huyo kwa jina la Mohamed Athumani Mjaila (85) ambaye alifariki dunia Julai 11 na kuzikwa siku iliyofuata katika makaburi yao ya ukoo katika Kijiji hicho. "Ni kweli tukio hilo limetokea Julai 18 majira ya asubuhi huko katika Kijiji cha Mgela kwenye makaburi ya familia ambako walikuta watu wamefukua na kundoka na kichwa," alisema. 

Kamanda alisema awali Wananchi waliona kaburi limefukuliwa wakahisi kwamba huenda watu hao wameondoka na mwili wote lakini walipofukua kujiridhisha, walikuta inekatwa kichwa ambacho waliondoka nacho na kubakisha mwili kwenye kaburi hilo.

Alisema familia na jeshi hilo wanahisi ni Imani za kishirikina lakini Polisi wameanzisha uchunguzi wa kuwasaka wahusika ili wawafikishe katika vyombo vya sheria.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii