Watatu wafariki na sita majeruhi kwa ajali Iringa

Watu watatu wamefariki dunia na wengine 6 wamejeruhiwa katika ajali ambayo imehusisha gari ya abiria lenye namba za usajili T 562 EBK aina ya Fuso Mini Bus inayomilikiwa na Khatibu Kihwelo likiendeshwa na dereva Akhan Mpagile (45) mkazi wa Njombe ambaye amefariki kwenye ajali hiyo. 

Akizungumza kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa ACP Allan Bukumbi amesema kuwa ajali hiyo imetokea July 18, 2025 saa 12 asubuhi kwenye kijiji cha Imalutwa Kata ya Lugalo, Tarafa ya Mazombe Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa katika barabara kuu ya Morogoro Iringa na kusababisha vifo vya watu watatu  na majeruhi 6 ambapo waliofariki ni dereva wa Minibus na wengine ni Alfred Mgaya mkazi wa Njombe ambaye ni utingo wa basi hilo na Feleschina Masigati (36) mkazi wa Imalutwa aliyekuwa abiria. 

ACP Bukumbi ameeleza kuwa gari hiyo ya abiria aina ya min Bus iligonga kwa nyuma gari lenye namba T857DVZ na Trela namba T460EAM aina ya Howo mali ya Glenrich Transportation Co Ltd lililokuwa likitokea Dar es salaam likiwa limebeba mzigo wa unga ambapo dereva wa Lori hilo alikimbia baada ya kutokea kwa ajali. 

Aidha ACP Bukumbi amesema Chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi kushindwa kulimudu gari lake na kugonga kwa nyuma gari lililokuwa limesimama mbele yake.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii