Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, amesema kuwa anapinga vikali vitendo vya utekaji na kudai kuwa dada yake alitekwa.
Kauli hiyo ameitoa kupitia video ya moja kwa moja (live) aliyoirusha kupitia ukurasa wake rasmi wa Facebook, akigusia pia masuala ya kisiasa na mwenendo wa chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika video hiyo, Polepole amesema tukio la utekaji wa dada yake limeacha doa la kihisia kwake binafsi na ni sehemu ya sababu zinazomfanya kuwa na msimamo mkali dhidi ya matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu.
Aidha, Polepole ambaye pia ni kada wa muda mrefu wa CCM, ameeleza kutoridhishwa kwake na namna baadhi ya masuala yanavyoendeshwa ndani ya chama hicho, akisema kuwa ni muda wa kujitathmini na kusikiliza sauti ya wananchi.
Kwa upande mwingine, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amethibitisha kupokea taarifa kutoka kwa dada wa Polepole kuhusu tukio hilo, akisema kuwa jalada la uchunguzi lilifunguliwa mara baada ya kupokea malalamiko hayo.