Watu watatu wamefariki dunia wakiwemo wanafunzi wawili wa kidato cha nne, kufuatia ajali ya barabarani iliyohusisha pikipiki yenye namba za usajili MC 534 DYX iliyokuwa ikiendeshwa na Baraka Sajio(22) iliyokuwa ikitoka Kihonda kuelekea Morogoro mjini, kugongana na lori lenye namba za usajili T 310 DQC lililokuwa linaendeshwa na Omary Juma(45) ambalo lilikuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Dodoma, katika eneo la Bima, Kata ya Mafisa, mkoani Morogoro, barabara kuu ya Morogoro–Dodoma.
Ajali hiyo imetokea leo Julai 18, 2025 majira ya asubuhi na kusababisha vifo vya watu watatu ambao ni Lusajo Mwang’onda(18) mwanafunzi wa kidato cha nne Morogoro Sekondari mkazi wa Kihonda Mkomola, Ghalib Omary(18) mwanafunzi wa kidato cha nne Morogoro Sekondari mkazi wa Kihonda Maghorofani na Baraka Sajio(22) dereva bodaboda mkazi wa Kihonda Maghorofani.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea huku chanzo cha ajali hiyo kikitajwa kuwa ni uzembe wa dereva wa bodaboda aliyekuwa akijaribu kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limewataka madereva wote kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, likitoa onyo kali kwa madereva wote wanaoendesha kwa uzembe kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.