Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limethibitisha kupokea taarifa za kutekwa na kurejeshwa kwa mwanamke aliyejitambulika kwa jina la Christina Hezroni Polepole Kinyangazi, mwenye umri wa miaka 52, mkazi wa Bahari Beach, mtaa wa Katumba, Kinondoni.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa leo na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro tukio hilo lilianza kuripotiwa kupitia mitandao ya kijamii mnamo Julai 17, 2025, ambapo mtu aliyejitambulisha kwa jina la Humphrey Polepole alidai kuwa dada yake alichukuliwa na watu wasiojulikana waliovamia nyumba yake kwa kuruka ukuta.
“Dada huyo alifika katika kituo cha Polisi Kawe na kutoa taarifa zinazohusiana na yeye kuchukuliwa na watu ambao hakuwafahamu na baadae walimrudisha nyumbani kwake jana hiyohiyo”, ameeleza Muliro.
Jeshi hilo limethibitisha kuwa linaendelea kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo kwa kushirikiana na wananchi pamoja na vyombo vingine vya usalama, huku likitoa wito kwa wananchi kuendelea kuwa watulivu wakati taratibu za uchunguzi zikiendelea.