Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei mpya za mafuta zitakazoanza kutumika Jumatano, Juni 4, huku gharama za bidhaa hizo zikipungua kidogo ikilinganishwa na mwezi uliopita.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, EWURA imesema kushuka kwa bei kimataifa katika soko la Ghuba ya Kiarabu pamoja na kushuka kwa thamani ya dola dhidi ya shilingi ya Tanzania kumechangia kushuka kwa bei za mafuta aina ya petroli, dizeli na mafuta ya taa. Bei ya FOB kwa petroli ilishuka kwa asilimia 0.9, dizeli kwa asilimia 3.4 na mafuta ya taa kwa asilimia 3.7
Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa wauzaji wa mafuta hawapaswi kuzidisha bei za kikomo zilizotangazwa na wanatakiwa kuonyesha bei waziwazi katika vituo vyao pamoja na kutoa risiti rasmi kwa kila muamala. EWURA imesema itachukua hatua za kisheria dhidi ya watakaokiuka masharti hayo.
Kampuni za mafuta zimeruhusiwa kuweka bei ya ushindani mradi hazizidi bei kikomo wala kushuka chini ya kiwango cha sakafu.