Serikali ya Marekani imefuta visa za takriban wanafunzi 300 wa kigeni kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na maandamano ya wanaounga mkono Palestina katika vyuo vikuu, hatua inayotajwa kuwa sehemu ya kampeni ya utawala wa Rais Donald Trump dhidi ya kile inachokiita chuki dhidi ya Israel.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alithibitisha hatua hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara yake nchini Guyana.
“Labda zaidi ya 300 kwa wakati huu,” alisema Rubio. “Tunafanya hivyo kila siku, kila ninapompata mmoja wa hawa vichaa.”
Serikali ya Marekani imekuwa ikichukua hatua kali dhidi ya wanafunzi wa kigeni wanaoshiriki maandamano yanayopinga hatua za Israel dhidi ya Wapalestina.
Hatua hizo zinajumuisha kufuta visa, kuwakamata baadhi ya waandamanaji, na kuzitaka taasisi za elimu ya juu kuwachukulia hatua wanafunzi wanaoendesha harakati zinazoelezwa kuwa chuki dhidi ya Wayahudi.
Kwa mujibu wa maafisa wa serikali, kufutwa kwa visa hizi kunalenga kudhibiti kuenea kwa kile wanachodai kuwa ni matamshi ya uchochezi katika vyuo vikuu.
Kisa cha hivi karibuni kinahusisha mwanafunzi wa shahada ya udaktari kutoka Uturuki aliyekuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Tufts, ambaye alikamatwa na maafisa wa uhamiaji.
Waziri Rubio alitetea kukamatwa kwake, akisisitiza kuwa Marekani haitaruhusu watu kutoka mataifa ya kigeni kuendesha harakati zinazoeneza chuki dhidi ya Israel katika vyuo vyake.
Hatua hii imezua mjadala mkubwa huku wanaharakati wa haki za binadamu na baadhi ya vyuo vikuu wakielezea wasiwasi wao kuhusu uhuru wa kujieleza.
Wanasema kuwa serikali ya Trump inatumia suala la chuki dhidi ya Wayahudi kama kisingizio cha kuwanyamazisha wale wanaoikosoa Israel.
Mashirika kama Amnesty International na Human Rights Watch yameitaka serikali ya Marekani kuheshimu haki ya wanafunzi kujieleza na kukusanyika kwa amani, yakisema kuwa hatua hii ni shambulio dhidi ya uhuru wa kitaaluma na haki za binadamu.