NCCR Mageuzi Yamteua Haji Ambar Khamis kuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania

Chama cha NCCR Mageuzi Machi 29, 2025, kimetangaza kumteua Haji Ambar Khamis kuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania na Joseph Roman Selasini kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2025.

Uteuzi wa wagombea hao umefanywa na mkutano Mkuu wa Chama hicho uliofanyika Katika ukumbi wa ST. Gasper Jijini Dodoma.

Katika hotuba zao za shukrani baada ya uteuzi, wagombea hao wamewaeleza wajumbe kwamba watajitahidi kufanya siasa za kistaarabu kwa kulinda na kudumisha tunu za taifa kama vile amani, upendo, na mshikamano.

Wamesisitiza umuhimu wa kushirikiana na vyama vyote vya siasa nchini katika kuhamasisha mageuzi na mabadiliko chanya ya kijamii, ikiwemo chama cha Mapinduzi (CCM).

Kadhalika wameeleza kwamba watakuwa na Sera za kulinda na kutunza Mazingira ili kudhibiti majanga ya mabadiliko ya Tabia Nchi ambayo yameendelea kuiathiri Nchi yetu.

Aidha Chama cha NCCR Mageuzi kimesisitiza kwamba kitashiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa 2025, na kimeonesha kujitolea kwa dhamira yake ya kukuza demokrasia, haki, na maendeleo endelevu kwa taifa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii