Burundi yatoa onyo dhidi ya shambulio lolote kutoka Rwanda

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye, amesema kuwa wamepata taarifa za kuaminika kuwa taifa la Rwanda linapanga kuishambulia Burundi.

Hata hivyo serikali ya Rwanda imekanusha vikali madai ya serikali ya Burundi.

''Matamshi ya Burundi ni ya kushangaza kwasababu idara za ulinzi za nchi hizi mbili zimekuwa zikikutana kujadili namna ya kulinda mipaka yao haswa wakati huu kuna mzozo Mashariki mwa DRC,''  msemaji wa serikali ya Rwanda Yolanda Makolo aeleza.

Ndayishimiye amesema Rwanda itakuwa imefanya kosa kubwa kuivamia Burundi kwa njia yoyote ile akisema Burundi itajibu kwa njia ya Kijeshi, na hivyo kuonya uwezekano wa kuzuka kwa vita vya kikanda.

Rais huyo wa Burundi amesema pia "hatutakubali kuchinjwa kama mbuzi, kama vile Wakongomani"

Serikali ya burundi tayari imetuma ujumbe kwa rais wa Rwanda Paul Kagame ili mchakato kwa kutekeleza makubaliano yao ya maridhiano ili kupunguza uhasama kati yao.

"Tumefanya mazungumzo na Rwanda kwa muda mrefu na tukakubaliana na ilipofika wakati wa utekelezaji, Rwanda ikasita" alisema Rais Ndayishimiye.

Burundi imeishutumu Rwanda kwa kuwapa hifadhi watu wanaoaminika walijaribu kufanya mapinduzi ya serikali nchini Burundi mwaka wa 2015. Aidha Burundi imedai kuwa utawala wa wa Rais Paul Kagame inawapa misaada waasi wa Red Tabara, ambao mara kwa mara hufanya mashambulizi ya kuvizia nchini Burundi kutoka Mashariki mwa DRC .

Amesema Burundi imejiandaa vilivyo kulinda mipaka yake na kamwe haitaruhusu uvamizi wa aina yoyote na kuishutumu, Rwanda kwa kufadhili makundi ya waasi yanayosababisha maafa Mashariki mwa Congo.

Mashambulizi ya hivi karibu kutoka kwa waasi wa Red Tabara, nchini Burundi, yalisababisha nchi hiyo kufunga mipaka yake na Rwanda.

Utawala wa Burundi umesema kuwa mchakato wa kuwakamata na kuwafungulia mashtaka viongozi wa waasi wa Red Tabara unaendelea na kuwa serikali haina nia yoyote ya kufanya mazungumzo nao. Rais Ndayishimiye amesema kuwa jukumu la serikali yake sasa ni kuwasaka waasi hao na kuwafikisha mahakamani.

Rais Ndayishimiye amesema Burundi haina nia yoyote ya kuvamia nchi nyingine au kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na hivyo inastahili kupewa heshima kama hiyo pia.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii