Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Rajabu Mabele ametoa wito kwa watu wote wanaoghushi vyeti vya mafunzo ya JKT kuacha kufanya hivyo na badala yake wajitokeze kupata mafunzo nafasi zinapotangazwa.
Pia ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuliwezesha Jeshi la Kujenga Taifa katika kuboresha miundombinu ya Vikosi na Makambi ya JKT.
Meja Jenerali Mabele ametoa shukrani hizo wakati akizindua Jengo la Ofisi Kuu ya kikosi cha Chita JKT pamoja na Bwalo la Maafisa alipofanya ziara ya kutembelea kikosi cha Chita JKT kilichopo Wilaya ya Kilombero Mkoa wa Morogoro tarehe 25 Machi 2025.
Meja Jenerali Mabele amefafanua kuwa, majengo hayo yamejengwa kwa kutumia fedha za maendeleo zinazotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Ulinzi.
Amesema Serikali imeendelea kujenga miundombinu mipya na kuboresha ya zamani ili kulijengea uwezo Jeshi la Kujenga Taifa kuchukua idadi kubwa ya Vijana wanaopatiwa Mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria na Kujitolea.