WALIMU wa Shule za Sekondari wanaofundisha masomo ya Sayansi na Hisabati,wametakiwa kutumia mbinu za kisasa zinazozingatia mabadiliko ya sayansi na teknolojia ili kuwasaidia wanafunzi kuyapenda masomo hayo na kuelewa mada ngumu kwa urahisi.
Mbinu hizo ni sehemu ya juhudi zinazowekwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari nchini (SEQUIP).
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tano kwa walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati yanayofanyika mkoani Singida katika Shule ya Sekondari Mwenge, Mratibu wa Kituo cha Mafunzo, Winchslaus Balige, amesema kuwa malengo ya mradi huo ni kuwawezesha walimu kutumia mbinu bora na za kisasa katika ufundishaji na ujifunzaji.
Amesema kwamba mbinu za ufundishaji watakazojifunza walimu zitahusisha namna ya kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati.
“Mafunzo haya endelevu ya walimu kazini yatasaidia walimu kufahamu namna ya kuandaa zana mbalimbali za kufundishia. Watafundishwa jinsi ya kutumia vishkwambi wakati wa kuandaa masomo kwa kuzingatia maagizo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye wakati wa kugawa vifaa hivyo kwa walimu aliwahimiza vikatumike kwa ufanisi ili kurahisisha kazi ya ufundishaji,” amesema Balige.
Mwenyekiti wa Wawezeshaji wa mafunzo hayo, Dk. Emmanuel Sulungu, ambaye pia ni Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Idara ya Fizikia, amewasisitiza walimu kubadilisha mbinu zao za ufundishaji baada ya mafunzo, ili kuwasaidia wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao.
Akifungua mafunzo hayo, Ofisa Taaluma Mkoa wa Singida, Lago Sillo, amewataka walimu wanaoshiriki mafunzo hayo kuyapa thamani ili yawanufaishe katika utekelezaji wa majukumu yao, kwa kuzingatia Sera ya Elimu ya mwaka 2014, Toleo la 2023, ambayo inasisitiza matumizi ya teknolojia katika ufundishaji.
Miongoni mwa walimu wanaoshiriki mafunzo hayo ni pamoja na Jesca Matezi kutoka Shule ya Sekondari Buhingo, Wilaya ya Chato, mkoani Geita, ambaye amesema anatarajia kufundishwa mbinu mpya za ufundishaji katika somo la Fizikia.
Amesema somo hilo linaogopwa na wanafunzi wengi, wakidhani ni gumu, lakini kupitia mafunzo atapata mbinu mpya za kisasa ambazo atazitumia ili kuwafanya wanafunzi walielewe somo na kulipenda.
“Ninayofuraha kupata fursa ya kushiriki mafunzo haya, yataniwezesha kuzalisha wanafunzi wengi watakaopenda Fizikia na kuisaidia nchi yangu kuwa na wanasayansi wengi, ambao wataweza kusaidia taifa katika nyanja mbalimbali,” amesema Mwalimu Jesca.
Mwalimu Victorian Dominic kutoka Shule ya Sekondari Dareda, mkoani Manyara, anayefundisha somo la Hisabati, alisema ana shauku kubwa ya kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu mtaala mpya, matumizi ya lugha ya Kiingereza katika ufundishaji wa Hisabati.
Bahati Kisaka, anayefundisha somo la Biolojia katika Shule ya Sekondari Mwinyi, mkoani Pwani, amesema kupitia mafunzo hayo atawasaidia wanafunzi wengi kuvutiwa na somo hilo.
Hassan Kalilo, anayefundisha somo la Kemia katika Shule ya Sekondari Isela, mkoani Shinyanga, ameishukuru Wizara kwa kuandaa mafunzo hayo, akidai kuwa yatawasaidia walimu kupata maarifa mapya yanayohusiana na mabadiliko ya kisasa na mahitaji ya dunia.
Walimu 950 kutoka mikoa 21 ya Tanzania Bara, wanaofundisha masomo ya Sayansi na Hisabati, wanashiriki katika mafunzo hayo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari nchini (SEQUIP).